Rais Jakaya Kikwete.
ZAKAYO PETER, MBEYA
Nakupongeza Mh. JK kwa kusimamia utekelezaji
wa ilani ya uchaguzi ya CCM, ila kabla hujaondoka madarakani naomba
ututimizie wananchi wa Kamsamba utujengee daraja la kutuunganisha na
wananchi wenzetu wa Mkoa wa Rukwa katika Mto Momba kama ulivyotuahidi
Oktoba 31, mwaka 2009 ulipofanya ziara ya kikazi huku kwetu.
ANDREA KAYOMBO, NJOMBE
Mh. Rais, hizi vurugu za Mbeya maeneo ya
Tunduma na Mwanjelwa hujazisikia maana ni shida kwa wanyonge wanashindwa
kufanya shughuli zao kwa ufasaha, kikubwa nakupongeza kwa kulifanya
taifa kuwa na utulivu na amani ila kama rais unayetoa madaraka ujue kuna
mambo ambayo yatakuja yavuruge amani hapo baadaye, kama hili kundi la
vijana wasomi wakati ajira bado ni ndoto na hata hao wanaojiita panya
road wamekosa ajira ndiyo maana wanafanya hayo.
NSAJIGWA EDWIN, MBEYA
Kwanza nikushukuru kwa uongozi bora
uliouonyesha ambao unaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa kiongozi ajaye,
ushauri wangu napenda ututafutie kiongozi bora kama ulivyo wewe kwa kuwa
huna makuu.
JOSHUA MWAKILONGA, DAR
Nakupongeza rais wangu kwa mazuri yote
uliyotufanyia Watanzania, japo umekumbana na mengi lakini kuna vijana
wengi hapa nchini ambao hawana ajira, ningeomba ulitazame kwa kina hili
wimbi kubwa la vijana wasiokuwa na shughuli maalum za kufanya ikibidi
waende Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wapate ajira.
SALMATA SAIDI, DAR
Shikamoo baba JK, mimi ni mnyonge lakini
tunakuomba uendeshe gurudumu sawasawa ili lisitokee tatizo lolote, ni
bora tukawa maskini lakini tunaamani, utulivu na umoja, na kusisitiza tu
uchague kiongozi aliye bora atakayefuata nyayo zako inabidi uwe makini
na vyama pinzani kuhakikisha tunakaa mbali na maswala ya vita.
PETER THOMAS, MARA
Nakushukuru kiongozi wetu kwa kuiongoza vizuri
nchi yetu katika nyanja mbalimbali, ni kweli hakuna kiongozi
aliyekamilika hivyo hata katika utendaji wako huwezi kutenda mazuri
asilimia 100, japo kuna mengi yanakusonga tupilia mbali hili la ajira
kwa vijana ni janga la taifa na pamoja na hilo nchi yetu hii tunajivunia
kutokana na kuishi kwa amani lakini hili swala la mauaji ya hawa ndugu
zetu Albino inabidi upambane nalo kwa juhudi zote na kuondokana nalo.
PIUS PATRIC, SHINYANGA
Nakupa pole na majukumu rais wangu, najua
si kazi ndogo kuliongoza taifa letu umejitahidi kulitumikia vyema taifa
hili kwa kipindi chote cha miaka kumi na tulikuzoea, kwa kuwa ni
kiongozi mnyenyekevu unayependa kucheka na watu japo wapo watakao kusema
vibaya, jitahidi kurekebisha yale mapungufu machache ambayo yapo ndani
ya uwezo wako kwa kipindi hiki kifupi ulichobakiza madarakani.
SHARIFA MDIRIKO, MTWARA
Binafsi sijavutiwa kabisa na uongozi wako
tangu ulipoingia madarakani mpaka sasa unakaribia kumaliza muda wako,
kwa kuwa kuna mambo mengi umeshindwa kuyatekeleza vile inavyostahiki na
sioni haja ya kuyataja, maana yapo wazi kwenye jamii kuna mambo mengi
yameendelea kuwa tatizo kwenye taifa hili kwa ujumla.
KASSIM MTWEVE, NJOMBE
JK umetusahau sana Kijiji cha Mdilidili
Wilaya ya Ludewa, ulisema ajira kwa vijana lakini mpaka leo kimya na
unakaribia kuondoka madarakani, tunakuomba uje kututembelea na
kututimizia angalau yale machache uliyotuahidi tuwe tumeambulia matunda
ya uongozi wako na kutuacha tukiwa na mioyo safi bila kinyongo kwa ahadi
ulizotupa.
DAUDI MPENZWA, MKURANGA
Nakupongeza rais wetu umetufanyia mambo
mengi makubwa Watanzania, umeingia kwenye orodha ya marais wanaopendwa
na wananchi, ila kuna jambo moja umetusahau sisi watu wenye matatizo ya
ulemavu katika Chama cha Viziwi Tanzania (Chavita) tunahitaji sana
faraja yako kiongozi wetu.
EMMANUEL RORYA, MARA
Kwa bahati mbaya Watanzania ni taifa pekee
duniani ambao hata ukiwafanyia jema gani hawaoni na pale utakapoondoka
madarakani ndiyo tutagundua umuhimu wako, tofauti na Baba wa Taifa,
Julius Nyerere hakuna atakayekumbukwa sana zaidi yako, tunaweza kukubeza
lakini tutakukumbuka sana kutokana na mengi mazuri uliyoyafanya kadiri
Mungu alivyokujalia, nikushauri tu uwe muangalifu kwa wagombea urais wa
CCM usielemee upande wowote ule na uwe makini sana ili chama
kisigawanyike.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni