MMILIKI WA BLOG HII

MMILIKI WA BLOG HII
TANGAZA NASI MATANGAZO YA KIJAMII BURE KUPITIA BLOG HII

Jumapili, 19 Aprili 2015

Nisaidieni mwanangu anateseka na ugonjwa wa ajabu'.


Mtoto  Abel Mlanda (15), mkazi wa Vikindu Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, anaomba msaada kutoka kwa watu mbalimbali ili aweze kupata fedha kwa ajili ya kupata matibabu ya ugonjwa unaomsumbua kwa kipindi cha miaka 12 na hali hiyo kusababisha vidole vyake vya miguuni na mikononi kulika. 
 
Akizungumza  Jumapili, baba mzazi wa mtoto huyo, Magnus Mlanda, alisema mtoto huyo ambaye ni wa kwanza kuzaliwa alianza na dalili za upele miguuni na ikadhaniwa kuwa ni ugonjwa wa fangasi.
 
"Mwaka 2003 mwanangu akiwa chekechea na umri wa miaka mitatu, ndipo alipoanza kupata upele miguuni tukiwa tunaishi mkoani Rukwa, na nilipompeleka hospitali walisema anasumbuliwa na fangasi,'' alisema.
 
Aliongeza kuwa, baada ya kuanza matibabu  ya fangasi ndipo mwaka 2006 kidole gumba kilikatika chenyewe baada ya nyama kulika.
 
Alisema mwaka 2007 aliamua kuja jijini Dar es Salaam na kwenda Hospitali ya Amana, ambapo  aliambiwa mtoto hali yake sio nzuri anatakiwa apelekwe Hospitali ya Muhimbili.
 
Alisema alilazwa kwa kipindi cha miezi saba Muhimbili, na kuambiwa huo ni ugonjwa sugu, hivyo akawa  anapata matibabu ya sindano na kusafishwa vidonda .
 
Alisema mwaka 2008 walirudi tena Muhimbili tatizo likaongezeka la kulika miguu na mifupa ambapo vidole vya miguuni viliendelea kukatika na baada ya tatizo hilo kuendelea kwenye vidole vya mkononi ndipo madaktari wakashauriana na kumwandikia barua ili aende India kwa ajili ya matibabu zaidi.
 
"Mwaka 2014 mwezi wa tatu tulienda India kwa ajili ya matibabu ambapo gharama zililipwa na serikali tulikaa kwa kipindi cha wiki tatu kwa matibabu na kisha kuruhusiwa,'' alisema.
 
Aliongeza kuwa hapo India walimpima na kuona kuwa ana tatizo la ganzi na dalili za ukoma ambapo alipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani na kupatiwa madawa ya miaka miwili ili aendelee kutumia.
 
Alisema pamoja na kupatiwa dawa hizo, bado hali ya mwanaye inaendelea kuwa mbaya na anaendelea kukatika vidole vya mikononi na kutoka nyama.
 
Aliongeza kuwa hivi sasa amejaribu kumpeleka katika kliniki nyingine ambapo ananunua dawa kwa Sh. 100,000 kiasi ambacho amesema hana uwezo wa kumudu ndiyo maana ameamua kujitokeza kwenye vyombo vya habari kuomba msaada wa hali na mali ili mtoto wake aweze kupona.
 
Alisema kwa sasa hana kazi maalum na anaishi kwa vibarua yeye na mke wake ambapo kidogo wanachokipata ndicho kinachowasaidia kupata mlo.
 
Aliongeza kuwa ugonjwa wa mwanaye unamfanya azidi kuishi maisha ya shida kutokana na kukosa lishe ya kumpatia mwanaye. Pia mtoto wake anashindwa kwenda shule kutokana na ugonjwa huo hali iliyomfanya aishie chekechea akiwa na miaka mitatu.

Aliomba mtu yeyote atakayeguswa na tatizo la mwanaye awasiliane naye kupitia simu ya mkononi namba 0657 140 172 au 0682 782 894.

 NA NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni