Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limeyapiga marufuku maandamano ya wafuasi na wanachama wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema) yaliyopangwa kufanyika leo, huku chama hicho kikisema yako pale pale.
Maandamano hayo yameandaliwa kwa ajili ya kushinikiza kutolewa kwa
taarifa za matumizi ya Sh. milioni 720 za mradi wa ujenzi wa stendi ya
mabasi ya Msamvu.
Wiki iliyopita Chadema kupitia kwa Mwenyekiti wake wa Wilaya ya
Morogoro, James Mkude, kilitangaza kufanya maandamano hayo hadi katika
uongozi wa Manispaa ya Morogoro kushinikiza Mbunge wa jimbo la Morogoro
Mjini, Abdulaziz Abood (CCM),
apewe taarifa za matumizi ya fedha za mradi wa ujenzi huo baada ya
kunyimwa na uongozi wa Manispaa wakati wa ziara yake ya kukagua mradi
huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema jana
kuwa taarifa aliyoitoa Mkuu wa Polisi wilaya ya Morogoro ambaye ndiye
mwenye dhamana ya kutoa ulinzi kufanyika ili maandamano hayo yafanyike
imeonyesha kuwa kuna viashiria vya uvunjifu wa amani endapo maandamano
hayo yataruhusiwa, hivyo yamepigwa marufuku.
“Nina copy (nakala) hapa nimeletewa na OCD wangu, kuwa maandamano
hayo hayaruhusiwi kutokana na uchunguzi wake aliofanya kuwa kuna
viashiria vya uvunjifu wa amani endapo yatafanyika, mimi sitaki
malumbano na viongozi wa kisiasa, naomba waheshimu utaratibu pamoja na
sheria zilizopo,” alisema.
Alisema kuwa siyo lazima kufanya maandamano kwa ajili ya
kushinikiza kupewa taarifa hizo za matumizi ya fedha za ujenzi wa stendi
hiyo bali ipo njia mbadala kwa viongozi hao wa Chadema ni kwenda kwa
uongozi wa Manispaa ya Morogoro au ule unaohusika kuomba kupatiwa
taarifa hizo ili kuwaeleza wananchi katika mikutano yao.
“Sisi kama Jeshi la Polisi tutahakikisha tunasimamia sheria kwa
kuwa tunajua maandamano yamepigwa marufuku, ninawataka Chadema kuheshimu
maamuzi yaliyotolewa kuhusu kutofanyika kwa maandamano hayo,” alisema
Kamanda Paul.
Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwenendo wa Bunge na Halmashauri wa
Chadema, Dk. Albanie Marcossy, alisema kuwa maandamano hayo yapo pale
pale kwa kuwa kisheria wao wanapaswa kutoa taarifa tu kwa jeshi hilo na
sio kuomba kibali.
Alisema kuwa wao hawaogopi polisi kuwafyatulia mabomu na kuwataka
waandae mabomu ya kutosha kwakuwa wao wanatetea maslahi ya wananchi
ambao wamekuwa wakikatwa kodi huku fedha hizo zikiliwa na wajanja
wachache.
Meneja wa mradi wa ujenzi wa kituo cha Msamvu Property Company
Limited, Stanley Mhapa, alisema hakuna ubadhilifu wa aina yoyote katika
mradi huo wa ujenzi wa stendi na taarifa za ukaguzi zipo wazi na kutaka
yoyote mwenye mashaka aende kupata ukweli wa matumizi ya fedha hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni