Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid.
Zaidi ya akinamama wajawazito 70 katika kituo cha Afya cha
Chikande, Manispaa ya Dodoma wameandamana hadi Hospitali ya Rufaa ya
mkoa wa Dodoma kulalamikia mambo mbalimbali.
Malalamiko yao ni pamoja na kujifungulia njiani kutokana na
kutembea umbali mrefu kwenda hospitali hiyo na baadhi yao kukataliwa
kufunguliwa geti na walinzi wa hospitali wanapojisikia uchungu.
Martha Masine, alisema wameamua kuandamana ili kuwasilisha kilio
chao kwa uongozi wa hospitali hiyo ili matatizo yao yatafutiwe ufumbuzi.
“Walinzi wa hospitali ya mkoa wamekuwa wakikataa kuwafungulia geti
akina mama wanaofika hospitalini hapo usiku wakitokea Chikande na
kusababisha baadhi ya wenzetu kujifungulia njiani na kuhatarisha maisha
ya mama na mtoto anayezaliwa,” alisema Masine.
Alisema wamekuwa wakipata shida sana kufika hospitali hapo usiku, ingawa kituo hicho kipo nyuma ya hospitali.
“Tunaposhikwa na uchungu tunatembea hata kama ni usiku ni hatari
kutokana na njia kuwa ni vichochoro hadi kufika General (hospitali
hiyo),” alisema.
Aidha, alisema wamekuwa wakisindikizana mmoja wao anaposhikwa na
uchungu, lakini wanapofika hospitalini walinzi wanagoma kufungua mageti
na kuwalazimu kurudi kituoni.
Alibainisha kwa nyakati mbili tofauti akiwa bado katika kituo hicho
ameshuhudia akina mama wawili kujifungulia njiani kwa kutembea umbali
mrefu kufuata huduma na mwingine kukataliwa na walinzi.
“Bado nipo katika kituo hiki nasubiria kujifungua, muda bado
haujafika, lakini jamani sisi tunapata shida walinzi wa General
wanapotukatalia kufungua mageti, huwa inatulazimu kuanza safari ya
kurudi kituoni na kuna siku tukiwa njiani mwenzetu akajifungua
tukamsaidia sisi tuliopo,” alisema Masine.
Rose Atanas ambaye yupo katika kituo hicho akisubiria kujifungua,
alisema changamoto nyingine ni kituo hicho kuzidiwa uwezo kutokana na
kupokea akina mama wengi kutoka vijiji mbalimbali vya Mkoa wa Dodoma.
“Kituoni kuna kinamama wengi kuzidi uwezo wake, kituo kina vitanda
15 na hadi sasa kuna akinamama zaidi ya mia moja hali inayotulazimu
kulala wawili wawili au watatu na wengine kulala chini na pia kuna
wadudu watambaao kama vile kunguni na papasi,” alisema Atanas.
Alisema mbali na mrundikano huo pia unahatarisha afya zao na unatishia kuambulizwa na magonjwa ya kuambukiza.
“Pia tuna vyakula vyetu na kujipikia wenyewe kutokana na chakula
tulichokuwa tukikipata kutoka hospitali ya mkoa kusitishwa bila ya
kuambiwa sababu ya kufanya hivyo.
“Hapa tupo zaidi ya 100 kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Dodoma
wengine tunalazimika kulala chini vitanda havitoshi, vyoo vyevyewe
matundu yapo mawili na mabafu mawili yaani tukianza kuoga ni foleni na
kwenda msalani ni foleni,” alisema Rose.
Akijibu malalamiko hayo, Muuguzi wa zamu katika hospitali hiyo,
Sista Cesilia Sanya, aliwaahidi akinamama hao kuwa suala la walinzi
kutofungua geti halitajirudia.
Hata hivyo, alisema hospitali imepokea malalamiko ya akina mama hao
na walinzi waliobainika kufanya vitendo hivyo watachukuliwa hatua.
Na Augusta Njoji
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni