Baraza la Vyama vya Siasa limevitaka vyama vyote vilivyopata mgawo wa nakala ya Katiba inayopendekezwa kuwagawia wanachama na wananchi badala ya kuendelea kuzifungia kwenye makabati ya vyama.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Peter Mziray, akizungumza na waandishi
wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema serikali ilitoa nakala ya
Katiba hizo ili vyama viweze kuwagawia wanachama wake ambao watapata
fursa ya kusoma na kufanya tathmini kulinganisha na Katiba ya sasa.
“Vyama vikifungia kwenye makabati nakala za katiba inayopendekezwa
vitakuwa haviwatendei haki wananchi na lengo la serikali litakuwa
halijafanikiwa,”alisema.
Mziray ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha APPT
Maendeleo, alisema wananchi wakisoma Katiba inayopendekezwa wataweza
kufanya maamuzi sahihi siku ya kupiga kura ya maoni ya kuikubali au
kuikataa katiba hiyo.
Alisema APPT Maendeleo imeanza kusambaza nakala hizo katika maeneo
mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ili kuonyesha mfano kwa vyama
vingine.
Vyama vyenye wabunge vilipewa nakala 15,000 za Katiba inayopendekezwa na visivyokuwa na wabunge nakala 5,000.
Serikali ilianza kusambaza nakala milioni mbili za Katiba
inayopendekezwa nchini kote Februari mwaka huu ili kuwawezesha wananchi
kuisoma na kushiriki katika kura ya maoni.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk.Asha Rose Migiro akisambaza katiba
hizo, alisema zipo kata zaidi ya 3,800 nchini kote na lengo la Serikali
ni kusambaza nakala 300 katika kila kata ambazo zitasambazwa kwenye
vijiji, vitongoji na mitaa kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wilaya na
Wakurugenzi wa Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni