Yanga imepata CD zinazoonyesha mechi kadhaa za hivi karibuni za wapinzani wao katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika, timu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, imeelezwa.
Yanga na ESS zitacheza mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Kombe
la Washindi kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi ijayo na kurudiana wiki
mbili baadaye Tunisia.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zimesema uongozi umepata
"mikanda ya video ya hivi karibuni ya Etoel du Sahel ambayo itamsaidia
kocha (Hans van der) Pluijm" katika maandalizi.
Pluijm alithibitisha habari hizo kutoka kwa kiongozi ambaye
hakupenda jina limeifadhiwa kwa sababu si msemaji wa klabu kwa kuwa ameanza kuwafuatilia wapinzani wao hao kwa
kuangalia michezo yao ya hivi karibuni.
Mholanzi huyo ambaye aliiwezesha Berekum Chelsea ya Ghana kucheza
robo-fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2012, alisema
anaifuatilia kwa karibu Etoile kwa sababu anajua kuwa ni moja ya vigogo
vya soka barani.
Pluijm alisema kuwa tayari ameshaanza mikakati na mipango ya kukabiliana na kuwashinda waarabu hao kwenye uwanja wa nyumbani.
"Nafahamu Etoel ni timu kubwa kimafanikio Afrika ukilinganisha na
timu yangu lakini siwahofii kwa sababu naamini nina kikosi kizuri na
ninataka kumaliza kazi kwenye uwanja wa nyumbani kabla ya kwenda
kurudiana nao kwao," alisema Pluijm.
Alisema kuwa mchezo huo wa Jumamosi umekuja wakati sahihi ili
kuthibitisha ubora na uimara wa Yanga ambayo imefika hatua hiyo baada ya
kuzitoa timu za BDF XI ya Botswana na Platinum ya Zimbabwe.
"Tunakabiliwa na mchezo wa ligi Jumapili (kesho) lakini nimeshaanza
mikakati na programu dhidi ya Etoel na kwa kweli nawashukuru viongozi
wa Yanga kwa ushirikiano wanaonipa kuelekea kwenye mchezo.
"Mimi nasema wana Yanga na Watanzania wote watulie kwa sababu
tumejipanga kuhakikisha tunaingia hatua ya kumi na sita bora na
tutamaliza kazi hapa nyumbani," aliongezea kusema Pluijm.
Yanga ilianza kwa kuifunga BDF IX 3-0 lakini ikachapwa 2-1 ugenini
kabla ya kuifunga Platinum 5-1 na kwenda kufungwa 1-0 kwenye mchezo wa
marudiano nchini Zimbabwe.
Mara ya mwisho Yanga kukutana na waarabu iliifunga Al Ahly ya Misri
1-0 kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika
chini ya Pluijm kwenye Uwanja wa Taifa mwaka jana lakini ikatolewa kwa
matuta ugenini baada ya sare ya 1-1.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni