Mabomu yarindima kituo cha mabasi ubungo, Serikali yasalimu amri, yaafikiana nao, Baadhi ya mabasi yalianza safari mchana.
Wakati Mgomo wa mabasi umetikisa nchi nzima, mabomu ya machozi na risasi za moto jana zilirindima katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani, Ubungo, jijini Dar es Salaam na kusababisha taharuki kwa mamia ya wasafiri waliokuwepo kituoni hapo wakisubiri hatma ya safari zao.
Taharuki hiyo ilitokana na madereva wa mabasi yaendayo mikoani
kugoma kufanya safari zao, baada ya serikali kuwataka kutimiza masharti
iliyowapa yakiwamo ya kwenda kusoma kila baada ya miaka mitatu
wanapokwenda kuhuisha leseni zao.
Hata hivyo, mgomo huo ulisitishwa saa 7 mchana na madereva kuanza
safari kuelekea mikoani, baada ya serikali kufuta sharti la kuwataka
madereva kurudi shule na utumiaji wa tochi barabarani.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, alilazimika kutoa tamko
hilo baada ya kikao chake na madereva na viongozi wengine wa serikali.
HALI KABLA YA KUTOLEWA TAMKO
Wakati wasafiri wakiwa katika hali ya sintofahamu, ghafla kikosi
cha kutuliza ghasia kilifika nje ya kituo hicho na kuanza kupiga mabomu
ya machozi yalisababisha baadhi ya wasafiri wakiwamo watoto kupoteza
fahamu na wengine kutapika.
Katika purukushani hizo, wananchi waliokuwa nje ya kituo hicho
wakiwamo abiria na wasindikizaji, walianza kujibu mapigo kwa kuwarushia
askari hao mawe na kuchoma moto matairi.
Mapambano hayo yaliyoanza saa 3:00 asubuhi na kudumu takribani saa
moja, yalitulia baada ya kikosi hicho kuongeza nguvu zaidi kwa kuleta
gari la maji ya washawasha pamoja na mengine yaliyokuwa na askari wenye
silaha za moto na mabomu ya machozi.
WANANCHI WAOKOTA MABOMU
Wakati jeshi hilo likipiga mabomu hayo, baadhi yalikuwa hayalipuki na kudondoka chini.
mwandish Jumamosi ilimshuhudia kijana mmoja aliyekuwa nje ya mlango
wa kutokea kituoni hapo, akiokota mabomu hayo na kuyaweka mfukoni kisha
kuingia nayo mtaani.
Mmoja wa askari waliokuwa wakiyarusha alipoulizwa na mwandishi wa
habari hizi, alisema kuwa endapo mtu huyo akiyatoboa yatalipuka na
kumletea madhara.
KAMANDA KOVA
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova,
aliwasili kituoni hapo huku akisindikizwa na magari yaliyokuwa
yamesheheni askari polisi na kupokelewa na madereva hao kwa wimbo
uliokuwa ukimtaka awaachie huru wale wote waliokamatwa baada ya
kusitisha safari.
Kamanda Kova alikubaliana na madereva hao na kuwatangazia kuwa,
amewaachia huru wale wote waliokamatwa maeneo tofauti jijini Dar es
Salaam na kwingineko na kuagiza ufanyike utaratibu wa kuwafikisha hapo.
Kabla ya tangazo hilo, jeshi hilo lilikuwa limeshaachia huru
viongozi wakuu ambao ni Mwenyekiti wa Muungano wa Umoja wa Vyama vya
madereva nchini, Clement Masanja, Katibu wa Chama cha Mabasi, Abdallah
Bubala, Katibu wa Umoja wa Madereva na Katibu wa Chama cha Malori,
Rashid Salehe na Mjumbe wa Baraza la Umoja wa Madereva, Moris Liumbi.
MADERAVA NA MAKONDAKTA WA DALADALA
Wengine ambao walikuwa hawajaachiwa ambao Kova alishinikizwa na
madereva hao atekeleze hilo ni pamoja na watu 20 wakiwamo madereva na
makondakta wa daladala waliokuwa wanashikiliwa kituo cha Buguruni.
Pia wapo madereva wa mabasi ya mikoani 25 waliokuwa wamekamatwa
wakati wakiwa safarini kuja Dar es Salaam wakitokea Morogoro na kiongozi
mmoja wa madereva wa mkoa wa Iringa.
Baada ya kauli ya Kova, ilipotimu saa 5:49 asubuhi baadhi ya wale
waliokuwa wanashikiliwa na jeshi hilo, waliwasili kituoni hapo huku
madereva wakiimba wimbo wa kumsifu mkuu huyo wa polisi Dar es Salaam.
Hata hivyo, licha ya jitihada hizo za jeshi la polisi za kuwaachia
huru watu hao, madereva hao walikuja na hoja nyingine ya kumtaka kamanda
Kova, kuwaleta viongozi wa serikali hapo ili wazungumze nao kuhusu kero
zao.
Kamanda Kova alichukua kipaza sauti na kuwaeleza kuwa, tayari
ameshawasiliana na Waziri wa Kazi na Ajira, Kabaka ambaye alikubali ombi
hilo.
KABAKA AWASILI
Saa 6:16 mchana Waziri Kabaka alifika akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki.
Viongozi wengine waliofika ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi,
Dk. Shaaban Mwinjaka na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
MADAI YA MSINGI YAKUBALIWA
Mkutano ulianza kwa Katibu Salehe kutaja madai ya msingi wanayotaka
utatuzi wake kuwa ni pamoja na madereva wawe na mikataba bora na
kupinga kitendo cha serikali cha kuwataka kwenda kusoma kila baada ya
miaka mitatu wanapokwenda kuhuhisha leseni zao.
Madai mengine ni ucheleweshwaji wa malori kwenye boda hususani ya
Tunduma ambapo hukaa zaidi ya siku 26 licha ya kulipiwa kila kitu
bandarini.
Salehe alitaja mengine kuwa ni sheria namba G 31 ya mwaka 2015
ambayo inazungumzia kuhusu faini ya Sh. 300,000 au kifungo cha miezi 21
kwa madereva wanapofanya makosa barabarani.
Alitaja madai mengine kuwa ni tamko la Mkufunzi wa Chuo cha Taifa
cha Usafirishaji (NIT) alilolitoa Machi 31, mwaka huu kuwa, madereva
wote waliopata leseni PSV sio mahiri hivyo hata wakirudi shule watapata
alama 5.
Alisema madai mengine ni kukinzana kwa ratiba ya Mamlaka ya Usafiri
wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) pamoja na ile ya jeshi la polisi
kuhusu mwendo na kufika eneo husika.
Pia alitaja dai la mwisho kuwa ni mikataba ambayo wamiliki wa magari wamekuwa hawawashirikishi wao.
Baada ya madai hayo kutajwa Waziri Kabaka alijaribu kujibu baadhi
ya hoja huku zile ambazo zinawakereketa wahusika kama lile la kwenda
kusoma na mikataba likibaki na kitendawili kilichosababisha, viongozi wa
madereva hao kufunguka na kutaka majibu.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Kabaka alilazimika kutangaza kuwa kwa niaba ya wizara ya uchukuzi, suala la kusoma limefutwa.
Pia aliwataka walipuuzie tamko la NIT kwa sababu halina nafasi wala halipo serikalini bali lilikuwa ni la mtu binafsi.
Kadhalika alisema hatma ya mikataba yao itapatiwa ufumbuzi kwenye
kikao kinachotarajiwa kufanyika Jumamosi ijayo ambacho kitahusisha
viongozi wa madereva na serikali.
Aliwaagiza wamiliki wa mabasi na malori kuhakikisha wanapofuatilia
mikataba ya madereva wao, waongozane na wahusika na kuacha ubabaishaji.
Naye, Kamanda Kova alitangaza kuwa, kuanzia sasa suala la tochi
zinazotumiwa barabarani na polisi limefutwa na kuwataka madereva wafuate
sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali.
Kuhusu ‘mabao’ ya ovyo yanayofanya na trafiki barabarani ambayo
madereva hao waliyalalamikia, Kamanda Kova aliwapa watu hao namba zake
za simu ili wanapokamatwa wampigie.
Kova alitangaza kuwa kuanzia sasa kituo cha ukaguzi kitakachotumika ni kile cha mizani pekee.
ABIRIA WANENA
Mwanafunzi wa Kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya
Weruweru, Doris Mayemba, amesemakuwa, wanafunzi 66 wa shule
hiyo wamekwama kituoni hapo baada ya mabasi hayo kugoma.
Kuhusu upigwaji wa mabomu, Mayemba alisema kimewasababishia mshtuko
na mwanafunzi mwezake Linda Salonga, alizirai lakini sasa anaendelea
vizuri.
MBAGALA
Mbagala, hali ilikuwa ngumu baada ya polisi kutumia mabomu ya
machozi kuwatawanya madereva na abiria waliokusanyika kituo cha mabasi
cha Mbagala Rangitatu.
Tukio hilo lilianza majira ya saa 3:15 asubuhi, baada ya kundi la
madereva na wapiga debe kuwashusha watu waliopanda magari na pikipiki
maarufu kama bodaboda waliokuwa wakitoa huduma ya usafiri.
Watu hao waliweka vizuizi vya mawe katika Barabara ya Kilwa, hatua ambayo ilisababisha msongamano wa magari.
Polisi ambao walitumia magari matatu na pikipiki nne walifika eneo
hilo mara moja na kuanza kutupa mabomu na kusababisha madereva na abiria
waliokuwa kwenye kituo hicho kukimbia hovyo.
Milio ya mabomu ilisikika kwa muda wa dakika 15 na kusababisha watu
kukimbilia kwenye maduka ya jirani na Hospitali ya Zakhem kwa ajili ya
kulinda usalama wao.
Polisi hao walionekana wakiranda barabarani kuhakikisha usalama wa eneo hilo unarejea.
Polisi walifanikiwa kudhibiti eneo hilo na vituo vingine vya
Mbagala Kizuiani, Kipati, sabasaba na Mtoni kitu ambacho baadhi ya
madereva wa magari madogo ya mizigo na pikipiki walitumia nafasi hiyo
kuanza kubeba abiria waliosongamana kwenye vituo hivyo.
Hali katika kituo cha Tandika ilikuwa na ukimya kufuatia magari
kutoonekana kituoni hapo,huku magari machache yanayokwenda maeneo ya
Yombo yalionekana yakiendelea kutoa huduma ya usafiri.
Hata hivyo, mmoja wa dereva ambaye hakutaka kutaja jina lake,
alisema wao hawakushiriki kwenye mgomo huo kutokana na magari yao
kutotambuliwa na Sumatra.
“Sisi hatuhusiki na migomo kwa sababu hata Sumatra wanasema
hawatutambui, tunaendelea kuwachukua abiria kama kawaida,” alisema
dereva huyo.
BAJAJ, BODABODA, MALORI YANEEMEKA
Abiria walilazimika kutembea kwa miguu kutoka kituo cha Ubungo hadi Mbezi wakitafuta usafiri wa mikoani bila mafanikio.
Mgomo huo wa madereva ulizusha vurugu na ngumi kati ya abiria na kikosi cha kuzuia magari katika kituo cha Ubungo.
Wakiongea abiria Selina Elisante, akiwa na wanawe
watano huku akibubujikwa na machozi alisema wametumia gharama kubwa
kujinunulia mahitaji ambayo hayakuwapo.
Stephen Mdemo alisema kuwa matatizo ya mgomo yaliandaliwa na jeshi
la polisi lilikuwa na taarifa na kuhoji kwa nini hatua hazikuchukuliwa
na kuwatesa abiria bila sababu.
Hali hiyo ya mgomo iliwanufaisha waendesha bodaboda na bajaji
ambapo walianzisha umoja wa aina yake kwa kupandisha nauli kati ya Sh.
1000 hadi Sh. 5000 kwa abiria mmoja.
Nauli kutoka Tegeta Nyuki hadi Mwenge ilikuwa Sh. 5,000 na Kimara hadi Ubungo, Sh. 4,000.
Bodaboda ilitoza Sh. 4,000 kwa safari moja bila kujali umbali.
Viongozi wa Madereva waliomba msaada wa polisi kutoa ulinzi kwa
magari yatakayosafirisha abiria kutoka jijini Dar es Salaam kwenda
mkoani, jambo ambalo polisi halikulipa umuhimu wake mpaka pale majanga
yalipotokea na kuanza kuchukua hatua ya kurusha mabomu yakutawanya
wananchi.
Madereva hao wanapinga sheria za usajili inayowataka wakitaka
kuongeza daraja kwenda chuoni kusoma kwa madai kuwa hawana uwezo
kutokana na mishahara yao kuwa kidogo. Isitoshe, wamiliki hao hawawezi
kuwavumilia mpaka wamalize kozi, wanahofia kukosa kazi kwa mmiliki
kuajiri dereva mwingine.
Athari ya mgomo huo ulisababisha wafanyakazi wengi kufika maeneo
yao ya kazi wakiwa wamechelewa au kutofika kabisa huku wengi wakibebwa
kwenye malori ya mchanga yaliyokuwa yakitoza nauli ya Sh. 1000 kutoka
Mbezi hadi Ubungo.
Wakati huo huo, abiria walijikuta katika wakati mgumu katika
masuala ya usafiri na kujikuta wakitumia gharama kubwa. Anna Kilemba
ambaye alikuwa anasubiri usafiri wa kwenda Posta, anasema kutokana na
usafiri kuwa wa shida ilimlazimu kupanda gari aina ya NOAH ambapo
alilipa Sh. 1,500.
Hata hivyo baadhi ya abiria wakipanda gari
ambazo zinatumika kubebea mizigo maarufu kwa jina la ‘Kirikuu’ kwa
kutangaziwa nauli ya Sh. 1,000.
Baadhi ya watu ambao walikuwa wanapeleka chakula kwa wagonjwa
hospitali ya Muhimbili walijikuta katika wakati mgumu huku wakichelewa
kutokana na kukosekana kwa usafiri.
Amina abdallah alisema licha ya kuchelewa kufika hospitalini hapo
lakini imemgharimu zaidi ya Sh.10,000 kulipia usafiri wa bodaboda wakati
huwa anatumia Sh. 800.
PWANI
Abiria zaidi ya 1000 wa mabasi yaliyokuwa yakitoka mikoani kwenda
kituo cha Ubungo Dar es Salaam, walikwama katika kituo cha mabasi Maili
moja mjini Kibaha baada ya kuhofia kupigwa kufuatia mgomo wa madereva.
Baadhi ya abiria walilsema kuwa pamoja na mgomo huo
kuisha baada ya mazungumzo kati ya madereva na serikali wameshindwa
kusafiri kutokana na kuchoka na muda kuisha.
“Nipo hapa tangu asubuhi saa 12, hadi saa saba ndio tunaona magari
yanaanza safari, sasa nimeshachoka na muda nao umeshaenda pia bajeti
yangu hairuhusu kusafiri nimeshapunguza nauli kwa kununua chakula,
alisema Said Haji abiria aliyekuwa katika kituo cha Mail moja mjini
Kibaha.
Mmiliki wa magari ya Smart Bus yanayofanya safari zake kati ya Dar
es Salaam-Tanga-Mombasa, Nuru Jumbe, alisema mgomo huo umewaathiri kwani
gari lake moja lililokuwa kituo cha mabasi Ubungo ilipigwa mawe na
ilivunjiwa kioo cha mbele na hivyo kumlazimu kuipeleka gereji kwa
gharama kubwa ambazo hakuzitegemea.
MWANZA
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga, jana aligomewa na
madereva wa mabasi ya kwenda mikoani katika kituo kikuu cha mabasi
Nyegezi jijini Mwanza, baada ya kuwalazimisha kusitisha mgomo wao na
kuanza safari.
Akizungumza na baadhi wasafiri, madereva na wamiliki wa baadhi ya
mabasi hayo katika kituo hicho, alisema madereva wanapaswa kuanza safari
kutokana na wamiliki kutotambua mgomo huo.
“Abiria ingieni ndani ya mabasi yenu kwa ajili ya kuanza safari,
polisi jipangeni sawa kwa ajili ya ukaguzi na madereva waanze na
safari…kuna abiria wenye matatizo mbali mbali hapa na kutakiwa kuwahi
waendako, sasa safari ianze huku serikali ikizungumza na viongozi wenu,”
alisema Konisaga.
Konisaga aliyefuatana na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza,
Japhet Lusingu, viongozi wa mamlaka ya usafiri wa nchi kavu na majini
(Sumatra) mkoa na mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Mwanza,
alisema madereva hawana haki ya kugoma kutokana na wamiliki wa magari
kutoutambua mgomo huo.
Miongoni mwa abiria walioshindwa kusafiri, Mwenge Soka, alisema
wanashangazwa kwa kukatiwa tiketi hadi asubuhi, lakini wakifahamu mabasi
hayo hayawezi kusafiri.
KIGOMA
Zaidi ya abiria 2000 walipigwa butwaa jana katika stendi mpya ya
Masanga eneo la Manispaa ya Kigoma/Ujiji bila kujua la kufanya baada ya
madereva wa mabasi mbalimbali kugoma kutoa huduma hiyo.
Akizungumza , dereva wa basi la Saratoga linalofanya
safari zake Kigoma hadi Dar es Salaam, Ositazi Ibrahimu (45) alisema
wameunga mgomo wa nchi nzima baada ya viongozi wao wa Chama ch Madereva
Tanzania kukamatwa kwa madai ya kuwatetea madereva wote Tanzania.
Abiria Laila Rashid (30) aliyekuwa amepanda basi la Saratoga
kutoka Kigoma kuelekea Tabora, alisema alitakiwa aonane na daktari saa
nane mchana lakini ameshindwa.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Madereva Mkoa wa Kigoma, Tunu Rashid, alisema “tatizo kubwa ni mfumo wa serikali.
Naye Mwalimu Ezekieli Kanyangwa, ambaye ni abiria wa basi la
Adventure lililokuwa likielekea Mpanda alisema kilichomshangaza wakati
ameenda kukata tiketi hakuambiwa kuwa kuna mgomo.
Kanyangwa alisema hadi saa tano asubuhi nauli hawajarudishiwa na
mgomo unaendelea hawajui la kufanya wala hakuna kiongozi yeyote aliyetoa
taarifa kuhusiana na mgomo huo.
MTWARA
Abiria wa mabasi yanayoenda sehemu mbali mbali wameshindwa kusafiri
kutokana na mgomo wa madereva kupinga amri ya serikali kuwataka kwenda
kusoma.
Katika kituo cha mabasi Mtwara idadi kubwa ya
mabasi ya kwenda mikoani yakiwa yameegeshwa huku abiria wakiwa hawajui
la kufanya ikiwa tayari walishalipia tiketi kwa ajili ya kusafiri.
Akizungumza kituoni hapo, Vaileti Nickolous ambaye alikuwa
akisafiri kuelekea Dar es Salaam, alisema mgomo huo umewaathiri kutokana
na wasafiri kupoteza muda na wengine walikuwa wanakwenda kwenye
matatizo.
“Wengine wanawahi maofisini, wengine wanasafiri kibiashara..sasa
kama mfanyabiashara amenunua biashara zake anatakiwa sasa akasafirishe
na biashara yenyewe kama matunda, kwa mgomo kama huu lazima atapata
hasara,” alieleza Violet.
MASASI
Abiria waliokusanyika katika stendi kuu ya mabasi wilayani Masasi
walisema mgomo huo umewaathiri ikiwemo mipango mbali mbali waliyojiwekea
katika shughuli zao za kila siku.
Walisema wameshangazwa na madereva hao kukatisha tiketi kutoka kwa
abiria wakati wakifahamu kuwa walikuwa na nia ya kufanya mgomo.
Juma Omari na Fatuma Justice kwa niaba ya abiria wengine wamesema
kuwa wanasafiri kwenda Dar es Salaam lakini walipofika stendi walikuta
abiria wengine wakiwa wamekusanyika makundi huku baadhi wakiwa wamekaa
ndani ya magari wasijue la kufanya.
mwandishi wetu alishuhudia pia madereva wa pikipiki za miguu mitatu
na zile bodaboda zikishiriki katika mgomo huo ambapo mji wa Masasi
ulionekana kimya baada ya vyombo hivyo kutokuwapo barabarani na wakazi
wa mji huo wakilazimika kutembea kwa miguu kwenda katika shughuli zao.
SONGEA
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, alipohojiwa kwa njia ya
simu alisema kuwa tatizo hilo la mgomo wa madereva linafahamika na
tayari amekutana na kamati yake ya ulinzi na usalama kwa lengo la
kuangalia tatizo lenyewe lilivyo kwa mkoa wa Ruvuma.
Meneja wa kampuni ya usafirishaji wa mabasi ya Super Feo Christian
Sanga alipoulizwa sababu ya kukatisha tiketi wakati mabasi hayatasafiri,
alisema mgomo wa madereva ni wa kihuni kwa kuwa hawakupewa taarifa kama
madereva wao hawatafanya kazi.
LINDI
Abiria waliofika kituo cha mabasi mjini hapa walipigwa na butwaa baada ya kutokuta gari hata moja kituoni.
Kaimu Afisa wa Sumatra mkoani Lindi, Mwasi Christian, alipotakiwa
kutoa ufafanuzi kuhusu mgomo huo, alisema yeye si msemaji wa mamlaka.
Abiria waliokwama kusafiri waliiambia NIPASHE kuwa wamesikitishwa
na kitendo hicho huku wakiwatupia lawama matajiri kwa kushindwa kuwapa
haki zao za msingi madereva wao.
MOROGORO
gari ndogo za abiria maarufu kama daladala zinazofanya safari zake
ndani ya mkoa wa Morogoro ziligoma kwa muda wa saa kumi jana na
kusababisha abiria kupata adha ya usafiri huku wengine wakilazimika
kupanda pikipiki na magari ya wazi ili kufika maeneo yao ya kazi na
shuleni.
Mgomo huo ulioanza saa 12 asubuhi hadi kufikia saa 9 alasiri yalipoanza kufanyakazi kama kawaida.
Akizungumzia hilo Kamanda wa Polisi mkoani hapa Leonard Paulo
alisema, jeshi hilo linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kufanya fujo
na kuleta uvunjifu wa amani mkoani hapa.
Kamanda huyo alisema watu hao walikamatwa jana aprili 10, saa 5
asubuhi katika eneo la Kihonda wakijaribu kuwazuia madereva wenzao wa
magari na pikipiki kuacha kuwabeba abiria waliokuwa vituoni kwa madai
kuwa wanaendeleza mgomo huo hadi hapo watakapopata suluhu.
MBEYA
Mgomo wa madereva uliokuwa umepangwa kufanyika jana nchi nzima
haukufanyika kama ilivyokusudiwa na badala yake shughuli za usafirishaji
ziliendelea kama kawaida katika maeneo yote.
mwandishi wetu ametembea vituo vyote vya mabasi na
kushuhudia magari ya kusafirisha abiria na mizigo yakiendelea na
shughuli zake kama kawaida.
Katika Kituo Kikuu cha Mabasi jijini Mbeya, mabasi ya kwenda
mikoani yaliondoka kuanzia saa 12:00 asubuhi kuelekea maeneo mbalimbali
kulingana na ratiba walizopangiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa
Mjini na Nchi Kavu (Sumatra).
*Taarifa hii imeandaliwa na Romana Mallya, Moshi Lusonzo, Beatrice Shayo,
Efracia Masawe, Agnes Temu, Margaret Malisa,Pwani Hamisi
Abdelehemani, Masasi, Emmanuel Lengwa, Mbeya, Joctan Ngelly Kigoma,
Daniel Mkate, Mwanza, Juma Mohamed, Mtwara, Gideon Mwakanosya, Songea,
Said Hamdani, Lindi, Christina Haule, Morogoro
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni