Tukio la kujiua kwa askari Polisi wa kituo cha polisi Sikonge, mkoani Tabora, mwenye namba H 3416 PC Charles Mkoyi (27), limechukua sura mpya, baada ya ndugu kueleza utata wa majeraha aliyonayo ndugu yao na malalamiko yaliyoelezwa na marehemu siku chache kabla ya kukutwa na umauti.
Wakizungumza jana wanandugu hao ambao hawakutaka kutaja majina yao , walidai kuwa kabla ya kifo chake kijana huyo alilalamika kunyanyaswa na mmoja wa viongozi wa kituo hicho (jina limehifadhiwa), ambaye aliwaeleza ndugu zake kuwa manyanyaso yalikuwapo tangu alipoingia kazini.
“Mtoto wetu ni muwazi kila linalotokea alimweleza mama yake, anamshauri kwa kumwambia tulia tunafanya utaratibu wa kukuhamisha, tuna jiuliza katoa wapi ujasiri wa kujiua?” alihoji na kuongeza:
“Baadhi ya malalamiko aliyotueleza ni kupangwa zamu zisizo na mpangilio, kwa mfano, anakesha kazini badala ya kupumzika anatakiwa kurudi tena kazini...muda mwingi alikuwa anachoka sana na hata alipolalamika hakuwahi kusikilizwa na kiongozi huyo.”
Alisema utata unaanza Kituo cha Polisi alichodaiwa alijipiga risasi kwa kuwa alitolewa haraka na kupelekwa Hospitali ya Mkoa, huku picha zilizopigwa kwa ajili ya kuonyeshwa familia na upelelezi, zikionyesha amekaa kwenye kiti akiwa amekumbatia silaha.
“Tunavyofahamu eneo lolote lenye tukio la mauaji kama hayo, mtu haruhusiwi kufika wala kusafishwa hadi zipigwe picha na hata ndugu waone, lakini inaonekana walimnyanyua na kumkalisha kwenye kiti na kumpiga picha, kwa muda mfupi palisafishwa na mwili ukapelekwa Hospitali ya Mkoa. Tunajiuliza haraka hiyo ya nini?” alihoji.
Walisema mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha matatu ambayo ni shingoni kwa nyuma kukiwa na tundu dogo, chini ya kidevu kuna jeraha kubwa, juu ya jicho alikuwa na mchubuko.
Alisema kinachozua utata zaidi ni jinsi Charles alivyojipiga risasi kwa kuwa inaonyesha risasi iliingilia nyuma na kutokea mbele ambako kulikuwa na mfumuko mkubwa na nyuma tundu dogo, jambo ambalo lina shaka kwa kuwa kwa uelewa wa kawaida anawezaje kujipiga risasi kisogoni.
Ndugu hao walidai baada ya kufika kwenye kituo hicho, walionyeshwa barua mbili zilizoandikwa na askari huyo, moja ikiwa ya kikazi na nyingine ya familia na kwamba walisomewa kiasi ya familia na ya kikazi haikusomwa na hawakupewa.
“Hata kama wamezichukua kwa ajili ya upelelezi, lakini kwa nini barua moja ya kikazi iwe siri kwa tukio tata kama hili…
wanachotueleza ndugu yetu alikataa lindo lakini iweje akatae wakati alikuwa amekwenda kazini siku hiyo?” alihoji mmoja wa wanandugu.
Alisema hadi sasa ndugu hawajapewa simu yake ya kiganjani, vitu vyake vingine alivyokuwa navyo, nguo zake na vitu vingine vilivyokuwa kwenye chumba chake na kwamba utaratibu wa kumzika haukuwa wa kuridhisha na walifanya haraka haraka, jambo ambalo linawafanya wahoji uharaka ulisababishwa na nini.
“Tunajua mwili wa askari unaposafirishwa wanabeba na vitu vyake vyote, wanajua alikuwa hajaoa, hana ndugu, wameacha vitu vyake vyote, kesho tunavunja matanga ndiyo siku ya kugawana nguo za marehemu, kwa mazingira haya tutagawana nini?” alihoji.
Walisema taarifa ya daktari inaeleza kuwa askari huyo alifariki dunia kutokana na matatizo kwenye ubongo.
Walielezwa kuwa kabla ya kukutwa na mauti majira ya jioni, Charles aliitwa kwenye kikao na baada ya kutoka alilia kutwa nzima na hata alipokwenda nyumbani na kubembelezwa na mpenzi wake, hakunyamaza na ilipofika jioni alirudi kazini na baadaye walielezwa uamuzi aliochukua.
Waliongeza kuwa hakukuwa na ukaribu wa polisi katika mazishi, alikuwa askari mwenzao lakini alizikwa kama raia wa kawaida.
Askari huyo alizikwa Aprili 5, mwaka huu katika makaburi ya Makuyuni, Manispaa ya Dodoma, aliajiriwa wilayani Sikonge, Julai, mwaka 2013, baada ya kuhitimu mafunzo katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA).
Alisema walionana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Suzana Kaganda, na kumueleza malalamiko yote na kuahidi kuyafanyia kazi.
Kamanda Kaganda akiongea kwa njia ya simu, alisema ndani ya Jeshi la Polisi kuna utaratibu wa kufikisha malalamiko yoyote yanayohusu askari wao.
“Waambie hao ndugu waje kuniona badala ya kulalamika kwenye vyombo vya habari,” alisema Kamanda Kaganda.
Askari huyo anadaiwa kujipiga risasi Aprili 4, mwaka huu, ndani ya Kituo cha Polisi Sikonge na ilielezwa kuwa marehemu hakuacha ujumbe wowote wa sababu za kujiua.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni