Hatimaye mashine 248 za kisasa za kuandikisha wapigakura katika daftari la kudumu la wapigakura kwa kutumia mfumo wa elektroniki wa Biometric Voters Registration (BVR) zimewasili nchini, ili kuongeza kasi ya mwenendo wa mchakato huo, ambao umekuwa wa kusuasua.
Kusuasua kwa mchakato huo ulioanza mkoani Njombe, Februari 23,
mwaka huu kabla ya kusimama, kunatokana na mashine 250 za awali za
kuandikisha wapigakura zilizokuwa zikitumika, kushindwa kufanikisha kazi
ya kuandikisha wapigakura.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Julius Mallaba (pichani), alithibitisha jana kuwasili kwa mashine hizo nchini.
“Mashine hizo zimeshawasili. Ziko Dar,” alisema Mallaba, ambaye
hata hivyo alikataa kueleza lini zimewasili alipotakiwa na waandishi jana
kujibu swali hilo.
Wiki iliyopita, akijibu maswali ya waandishi baada ya kutangaza
kuahirishwa kwa kura ya maoni hadi itakapotangazwa tena, kuhusu idadi ya
mashine, ambazo zimewasili, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva,
alisema walitarajia kupata 248 siku yoyote kuanzia siku hiyo, ambazo
zitatumika kwenye mikoa minne.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Iringa, Ruvuma, Mtwara na Lindi na kuwa ratiba yake ingetolewa hivi karibuni.
Jaji Lubuva alisema mashine nyingine 1,600 zitawasili wakati wowote
na kwamba serikali imetoa Dola za Marekani milioni 72 (Sh. bilioni
133).
Kuwasili kwa mashine hizo, kunaifanya Nec kupokea mashine 2,098,
huku ikisubiri mashine 5,902, ili kukamilisha 8,000 zinazotakiwa.
Alisema vifaa hivyo vinanunuliwa na serikali kupitia kampuni ya
Lithotech Export ya Afrika Kusini, ambayo imeingia mkataba na Nec na
inaviagiza China.
Jaji Lubuva alisema uandikishaji unaendelea mkoani Njombe na
utakamilika Aprili 18, mwaka huu na vifaa (BVR Kits 250) zilizokuwa
zinatumika zitatumika katika mikoa itakayofuata. Alisema vifaa hivyo
vinanunuliwa na serikali kupitia kampuni ya Lithotech Export ya Afrika
Kusini, ambayo imeingia mkataba na Nec na inaviagiza China.
Taarifa zilizopatikana ndani ya Nec zinaeleza kuwa kampuni hiyo
ndiyo inayotoa muundo wa ndani (Soft Ware) ya mashine hizo na kwamba
utengenezaji wa mashine moja na kuweka vifaa vyote muhimu inachukua wiki
sita. Uandikishaji wapiga kura mkoani Njombe ulianza Februari 23, mwaka
huu, na hadi kukamilika Aprili 18, mwaka huu, utakuwa umetumia siku 45,
ukitoa siku za sikukuu na Jumapili.
Aidha, Nec ilisema ina uhakika wa kuandikisha wapigakura katika
daftari hilo hadi Julai, mwaka huu, na kwamba jiji la Dar es Salaam na
Zanzibar, itakuwa ya mwisho ili kuwezesha vifaa vyote 8,000 kutumika kwa
pamoja.
Jaji Lubuva alisema Nec iliomba vifaa Kenya na Nigeria, lakini
ilishindikana kwa maelezo kuwa vinatumika katika ngazi za serikali za
mitaa, na kwamba kuomba vifaa nje ni utaratibu wa kawaida kwa nchi za
Kusini mwa Jagwa la Sahara.
“Nchi za Malawi na kwingine zinakuja kujifunza kwetu, hapa kwetu
tatizo kubwa ni viongozi na siku zote Nabii hakubaliki kwao,” alisema
Jaji Lubuva.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni