Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akisisitiza jambo wakati
wa uzinduzi wa program maalum ya kutumia mbwa kudhibiti dawa za kulevya
na wizi wa pembe za ndovu jijini Dar es Salaam juzi.
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Idara ya Forodha na Ulinzi
wa Mipaka ya Marekani, imezindua program ya uimarishaji ulinzi katika
Bandari ya Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kwa
kutumia mbwa maalum kubaini dawa za kulevya na pembe za ndovu.
Wizara za Uchukuzi, Mambo ya Ndani na Maliasili na Utalii, ndizo zitakazohusika na program hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema jijini Dar
es Salaam juzi kuwa program hiyo inalenga kuimarisha ulinzi katika
maeneo hayo kwa kuanzia ili kupambana na wasafirishaji wa dawa za
kulevya na pembe za ndovu.
Chini ya mpango huo, Polisi wa Tanzania watapatiwa mafunzo nchini
Marekani ya kutumia mbwa maalum katika maeneo hayo ifikapo Septemba,
mwaka huu.
Waziri Nyalandu alisema dhamira ya serikali ni kuwa na ulinzi wa
namna hiyo katika mipaka yote ya nchi kuhakikisha taifa linakuwa salama
kutokana na uharibifu unaofanywa na watu wasio na mapenzi mema na taifa
lao.
Kamishina wa Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani, Gil
Kerlikowske, kwa upande wake alisema baada ya kupatiwa mafunzo katika
vyuo vya idara hiyo, Polisi wa Tanzania watarejea nchini wakiwa na mbwa
hao tayari kwa kuanza kazi ya kupambana na wasafirishaji haramu wa dawa
za kulevya na bidhaa zitokanazo na wanyamapori. “Program za kutumia mbwa
hawa maalum, huongeza kwa kiwango kikubwa uwezo wa bandari na viwanja
vya ndege kubaini bidhaa haramu zinazoingizwa au kutolewa nchini,”
alifafanua.
Ni mara ya kwanza katika historia ya idara hiyo kuwezesha matumizi ya mbwa katika kubaini pembe za ndovu.
Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia Miundombinu katika
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Aloyce Matei, alisema suala la
ulinzi na usalama, ni kati ya vipaumbele vikubwa vya mamlaka hiyo.
“Tunakaribisha sana program hii katika bandari yetu,” alisema Matei aliyemwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu TPA, Awadh Massawe.
Baada ya mafunzo hayo, wataletwa mbwa maalum wanne nchini; wawili
Bandari ya Dar es Salaam na wengine idadi kama hiyo Uwanja wa Ndege.
Matei aliishukuru Serikali ya Marekani kwa msaada huo wa kutoa utaalam kwa askari wa Tanzania ili kudhibiti uhalifu hapa nchini.
Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Virginia Blaser, alisema uzinduzi
huo ni matunda ya ushirikiano wa nchi hizo mbili wa muda mrefu katika
masuala mbalimbali yakiwamo ya kiuchumi.
“Program hii tunayoizindua leo (jana), ni mfano mzuri wa mafanikio
tunayoyapata pale ambapo wahusika wote tunashirikiana,” alisema.
na mwandish wetu
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni