Migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu iliyoanza juzi kuishinikiza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwalipa fedha za kujikimu, sasa imesambaa nchi nzima.
Jeshi la Polisi Wilaya ya Temeke jana lilitumia mabomu ya machozi
kuwatawanya wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (Duce) cha Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam waliokuwa wamekusanyika katika eneo la chuo
hicho kwa nia ya kufanya mgomo na maandamano.
Tukio hilo lilitokea jana saa 2.00 asubuhi, baada ya polisi kufika
katika eneo hilo wakiwa na silaha za moto na mabomu ya machozi.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Bugemwe Melkizedeki, alithibitisha wanafunzi hao kutaka kufanya mgomo.
Hata hivyo, alisema yeye pamoja na viongozi wengine wa serikali ya wanafunzi wakati mgomo huo ukiandaliwa kufanyika.
Alisema wakati huo yeye na viongozi wenzake walikuwa benki wakifuatilia malipo hayo.
Melkizedeki alisema hadi kufikia saa 4.00 asubuhi jana, wanafunzi
wote 3,500 walikuwa wameingiziwa fedha hizo, ambazo ni Sh. bilioni 1.3.
Alisema katika tukio hilo, wanafunzi nane walikamatwa na polisi,
ambao walipelekwa katika kituo cha polisi Chang’ombe kabla ya kuachiwa
kwa dhamana.
Miongoni mwa wanafunzi waliokamatwa, ni pamoja na Esau Meshack,
anayesoma Kitivo cha Ualimu, ambaye alisema mgomo huo umeathiri ratiba
nzima ya mtihani.
Alisema wakati mgomo huo unafanyika, alikuwa anaingia kwenye mtihani ndipo yeye na wenzake walipokamatwa na polisi.
Meshack alisema walifikishwa katika kituo hicho cha polisi, ambako
walipekuliwa, huku wakipigwa virungu, makofi kwenye masikio na
kudhalilishwa kwa kuvuliwa nguo.
Wakati hayo yakijiri, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na
Teknolojia cha Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam, Kitivo cha Ualimu
wa mwaka wa kwanza wa masomo, wamepanga kufanya maandamano leo. Tofauti
na wenzao wa Duce, maandamano hayo yanalenga kushinikiza kufunguliwa
kitivo hicho chenye wanafunzi zaidi ya 400 baada ya kufungwa kutokana na
kudai fedha za kujikimu.
Mwanafunzi wa Sayansi ya Ualimu wa Hesabu katika chuo hicho, Mayagi
Mustaph, alisema zaidi ya wanafunzi 400 wanashindwa kuingia darasani
kutokana na chuo kufungwa.
Waziri wa Fedha wa Serikali ya Wanafunzi hao, Joseph Jingu,
alipoulizwa kuhusiana na hilo, alisema wao kama serikali ya wanafunzi
waliuomba uongozi wa chuo kukifungua kitivo ili kuruhusu wanafunzi
kuendelea na masomo ifikapo Jumatatu ijayo.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) jana waliandamana
kuishinikiza HESLB kuwapa fedha hizo, ambazo wanadai zimecheleweshwa
muda mrefu na hivyo kuwafanya waishi katika mazingira magumu.
NIPASHE ilishuhudia wanafunzi hao wakitaka kuandamana chuoni hapo,
huku wakitamka kuwa kama wasingeingiziwa fedha jana, lazima waandamane
kuelekea kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa.
Askari wa Jeshi la Polisi walionekana wakirandaranda maeneo ya
chuo, kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 6.30 mchana wakiwa na silaha
mbalimbali, yakiwamo maji ya kuwasha, mabomu ya machozi na risasi za
moto.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Anjelina Mabula, aliwataka wanafunzi hao
kutoandamana, kwani suala lao linafuatiliwa kwa karibu na HESLB.
Kuhusu wanafunzi 89 wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) waliokamatwa na
polisi juzi na kushikiliwa katika kituo cha polisi cha wilaya mkoani
humo, Kamanda Mungi alisema wameachiwa kwa dhamana.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) wamegoma kushinikiza
serikali kupatiwa fedha hizo pamoja na kulalamika kukatwa fedha nyingi
kwa ajili ya Bima ya Afya.
Mgomo huo ulianza juzi usiku na kuendelea hadi jana kwa wanafunzi
wa Kitivo cha Elimu, Kozi Maalumu kwa ajili ya walimu wa masomo ya
sayansi na hisabati pamoja na Kitivo cha Sanaa ya Lugha na Sayansi ya
Jamii.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya viongozi waliotumwa na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kusikiliza madai yao, wanafunzi hao walisema
wanashindwa kuingia madarasani kutokana na hali ngumu waliyo nayo.
Waziri wa Mikopo wa Serikali ya Wanafunzi katika Kitivo cha Elimu,
Mpandalume Simon, alitaja sababu za mgomo huo kuwa ni kuishinikiza
serikali kusikiliza kilio chao cha kucheleweshewa fedha hizo.
Alitaja madai mengine kuwa ni kukatwa Sh. 100,000, lakini vyuo
vikuu vingine wanalipa Sh. 50,400 kwa ajili ya huduma ya bima ya afya.
Akizungumza na wanafunzi hao, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa,
alisema serikali imesikia kilio chao na ndio maana waziri mkuu
aliwatuma kuwasikiliza kutokana na yeye kubanwa na majukumu ya
kiserikali bungeni.
“Kabla ya kuonana na nyie tumepita utawala wa chuo na
wamethibitisha juu ya malalamiko yenu na wanasubiri fedha zikishafika,
watahakikisha ifikapo Jumatatu zitakuwa tayari chuo,” alisema Galawa.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Stephen Kebwe, alisema
amefika na viongozi wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ili kusikiliza malalamiko hayo.
Hata hivyo, baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao walijikuta
katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na wanafunzi na kulazimika
kukatisha mazungumzo bila kufikia mwafaka wakidai hawawataki, wanamtaka
waziri mkuu mwenyewe.
Imeandikwa na Frank Monyo, Dar; George Tarimo, Iringa na Ibrahim Joseph, Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni