Wakati uandikishaji wapigakura katika daftari la kudumu la wapigakura kwa kutumia mfumo mpya ya Biometric Voters Registration (BVR) ukianza leo jijini Mbeya, mchakato huo utaanza mkoani Dodoma kesho.
Awali, mchakato huo ulipangwa kuanza leo mkoani humo, lakini
ulishindikana kutokana na waandikishaji wa ngazi mbalimbali kuchelewa
kupata mafunzo.
Mratibu wa Uandikishaji mkoani humo, Paulo Ngusa, alisema utoaji
mafunzo ya uandikishaji kwa ngazi ya maafisa waandikishaji wasaidizi na
maafisa uchaguzi wa halmashauri kwa mkoa wa Dodoma yalifanyika Jumatatu
na Jumanne, wiki iliyopita na kwamba, ndicho kilikuwa kitu cha kwanza.
Alisema baada ya kupata mafunzo, maafisa hao walienda katika wilaya
zao na kuanza kutoa mafunzo kwa ngazi ya maafisa waandikishaji
wasaidizi katika ngazi ya kata, ambayo yalifanyika Alhamisi na Ijumaa
wiki iliyopita.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Isdory
Mwalongo, alisema mchakato huo kwa wilaya yake utaanza Mei 21, mwaka
huu, kutokana na kuchelewa kupata mafunzo.
MBEYA
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Mussa Zungiza,
alisema maandalizi ya uandikishaji wapigakura yamekamilika na kwa hiyo
mchakato huo utaanza leo.
Alisema waandikishaji 430 tayari wamepewa mafunzo ya namna ya
kuandikisha wapigakura kwa mfumo huo na kwamba, ofisi yake imejipanga
kuhakikisha mchakato unakamilika bila matatizo.
“Tumekuwa tukitoa mafunzo kwa waandikishaji wapigakura wapatao 430
na hivi leo (jana) tunafunga mafunzo tukiwa tumejiridhisha kuwa
wataifanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa,” alisema Zungiza.
Alisema mchakato huo katika halmashauri hiyo utafanyika kwa awamu
tatu; ya kwanza ambayo inaanza leo itakuwa kwenye kata 10 zenye vituo 65
vya kuandikishia wapigakura.
Na Augusta Njoji
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni