Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, amewataka vijana kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Afrika na China kwani ndiyo nchi pekee duniani ambayo imeonyesha kuwa ni rafiki wa kweli wa Bara la Afrika.
Rais Mugabe alitoa wito huo jijini Arusha jana, alipokuwa akifungua Kongamano la Viongozi wa Vijana wa Afrika na China.
Kongamano hilo linashirikisha washiriki 4,000 kutoka mataifa 40
ya Afrika likiwa na lengo la kujadili changamoto zinazowakabili Vijana
kwenye ulimwengu wa kibepari na namna bora ya kuvutia wawekezaji kuja
kuwekeza Afrika.
Alisema mahusiano kati ya Afrika na China yalianza muda mrefu na yataendelea kwa vizazi vijavyo.
Rais Mugabe alisisitiza kwamba China ni rafiki wa kweli wa Afrika
na urafiki huu utaendelea kudumishwa na kuuendelezwa kwa faida ya vizazi
vijavyo.
Mugabe aliisifia Serikali ya China kwa kusaidia Bara la Afrika tangu harakati za ukombozi hadi sasa.
Mugabe amewaambia vijana hao kuwa China bado inaendeleza harakati
zake za kusaidia Bara la Afrika katika utekelezaji wa programu
mbalimbali za maendeleo, kiuchumi na kijamii mchango ambao watu wa
Afrika na hususan Vijana wanapaswa kuuthamini.
Alisema China iliisaidia Tanzania na Zambia wakati wa ujenzi wa
reli ya Uhuru (Tazara), ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam
kwenda Kapiri Mposhi, Zambia (Tazama).
Pia China ilisaidia ujenzi wa mradi wa kiwanda cha urafiki pamoja
na mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira mkoani Mbeya pamoja na uanzishaji
wa mradi wa kilimo cha mpunga Mbarali.
Alisema nchi hiyo imesaidia miradi mingi barani Afrika
Aliwataka Vijana wa Afrika na China kuimarisha ushirikiano kati ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Kikomunist cha Watu wa China
(CPC).
Alisema Afrika bado inakabiliwa na changamoto nyingi hususan suala
la ukosefu wa ajira kwa vijana hivyo kongamano hilo litafute njia za
kupata ufumbuzi wa namna ya kuwawezesha vijana kupata ajira kwa
kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayowawezesha vijana wa Afrika
kujiajiri.
Na Cynthia Mwilolezi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni