Wanaharakati nchini wamesema rais ajaye anaweza kuwa mwanamke
kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo wingi na hamasa waliyonayo wanawake
katika upigaji kura.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema ingawa
wanatambua uchaguzi ni mapambano, wanaamini kama wanawake na jamii
itakubali mabadiliko, nchi itaongozwa na rais mwanamke.
Wanaharakati hao kutoka vyama vya Umoja wa
Wanawake Wanasiasa (Ulingo), Mtandao wa Jinsia Tanzania, (TGNP), Kigoda
cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) walisema hakuna
kinachoshindikana kama wanawake wataamua.
Ulingo
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wanasiasa Tanzania
(Ulingo), Anna Abdallah alisema, baada ya wanawake kuangaliwa kama
kundi duni katika nyanja za siasa kwa muda mrefu, sasa ni zamu yao
kujitokeza wagombee nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwamo ya urais.
“Lengo letu sisi ni mwanamke kujitokeza,
akijitokeza tutamuunga mkono kwa umoja wetu bila kujali anatoka chama
gani cha siasa,” alisema mwenyekiti huyo aliyeeleza kuwa jamii ya sasa
ina imani kubwa na mwanamke.
Aliongoza “Iwapo wanawake watafanya kile
tunachotaka , kwa maana ya kuwaunga mkono wagombea, kupiga kura, wakati
wa kupata rais mwanamke umefika. Hilo halina ubishi na linawezekana.”
Anna alitaja sababu nyingine za kuwashawishi wanawake wajitokeze
kugombea urais kuwa ni kuongezeka kwa uelewa wa wanawake katika masuala
ya siasa.
TGNP
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania, (TGNP),
Lilian Liundi alisema wanawake kuwa viongozi siyo ajabu kwani tayari
wameshafanya hivyo katika nafasi mbalimbali. Isipokuwa wanahitaji
kuungwa mkono katika nafasi za kisiasa.
Alisema mtandao huo utamuunga mkono mwanamke
yeyote atakayeonyesha nia ya kugombea bila kuangalia itikadi ya chama
anachotoka, huku ukiamini kuwa wanawake wanaweza kufanya vizuri zaidi
wanapopata nafasi.
“Japokuwa historia inaonyesha wanafanya vizuri,
tunahitaji kuwaunga mkono kwa nia thabiti ili wakalete mabadiliko ya
kweli, ” alisema Liundi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni