Imeelezwa kuwa kitendo cha wananchi wengi kukosa elimu ya kiroho inachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe katika mkoa wa Shinyanga.
Hayo yamesemwa na katibu wa Chama Cha Watu wenye Ulemavu wa ngozi katika wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Seif Rashid wakati wa majadiliano maalum na waandishi wa habari yaliyoandaliwa na TGNP Mtandao yaliyofanyika mjini Shinyanga.
Rashid amesema vitendo vya mauaji vinafanywa na watu
wasiokuwa na hofu ya mungu hivyo kuzitaka taasisi za kidini kuwapa elimu ya
kiroho ili kutokomeza mauaji katika jamii.
Amesema kitendo cha wananchi kukosa hofu ya mungu ndicho
kinawafanya wakimbilie kwa waganga wa kienyeji wakiamini kuwa watatatuliwa
matatizo yao.
Amesema mbali na kukosa elimu ya kiroho,wananchi wengi
hawana elimu dunia,matokeo yake wanawaamini waganga wa jadi kupitia ramli
zao,vitendo ambavyo vinachangia mauaji ya watu wasio na hatia kwani
waganga wengi wa jadi wanafanya ramli
chonganishi.
Nao baadhi ya wananchi wa
wilaya ya Kishapu waliohudhuria majadiliano hayo wamesema changamoto iliyopo
wilayani Kishapu ni ubaguzi wa rangi katika jamiii ambapo watoto wenye rangi
nyeupe wanaonekana kuwa na thamani zaidi ya watoto wenye rangi nyeusi.
Wamesema hivi sasa watoto wenye rangi nyeupe wanalazimishwa
kuolewa ili wazazi wapate ng’ombe kuanzia 25-35 na wenye rangi nyeusi wakiolewa
kwa ng’ombe 4 hadi 10 huku wengine wakikatishwa masomo yao.
Naye afisa program,utafiti na uchambuzi kutoka TGNP Mtandao
Deogratius Temba amekemea kitendo cha watoto kuachishwa masomo ili waolewe na ameitaka
jamii kubadilika na kuacha kubagua watoto kwani kufanya hivyo ni kuendeleza vitendo
vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Na NEEMA RUBEN
----mwisho--
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni