MMILIKI WA BLOG HII

MMILIKI WA BLOG HII
TANGAZA NASI MATANGAZO YA KIJAMII BURE KUPITIA BLOG HII

Jumatano, 17 Juni 2015

Mufti mpya ni kati ya hawa.


Rais Jakaya Kikwete ameongoza mazishi ya Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shabaan bin Simba yaliyofanyika katika makaburi ya Nguzo Nane, mjini Shinyanga, huku Baraza la Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata)  likianza mchakato wa kumpata mrithi wake.
Mufti Simba ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi katika hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam, mazishi yake yalifanyika jana na kuhudhuriwa na maelfu ya watu wakiwamo viongozi wa dini, viongozi wa serikali na wa vyama vya siasa.
Awali kabla ya mazishi hayo ilifanyika swala ya kuombea mwili wa marehemu katika msikiti wa Majengo uliopo mjini Shinyanga.
WAWANIA URAIS WAHUDHURIA
Pamoja na Rais Kikwete mazishi hayo pia yalihudhuriwa na wagombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Allynassoro Rufunga, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salim na viongozi wengine wa chama na serikali.
MCHAKATO WA KUMRITHI WAANZA
WAKATI mazishi ya kiongozi wa kidini yakifanyika, Bakwata limeanza mchakato wa kumpata mrithi wa nafasi yake.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mohamed Mhinga, alisema Baraza la Ulamaa litakaa na kuteua kiongozi atakayekaimu nafasi hiyo kwa muda siku 90 kabla ya kufanyika uchaguzi.
“Baraza la Ulamaa baada ya mazishi litamteua kiongozi atakayekaimu  kwa muda wa siku 90 huku likiandaa utaratibu wa kufanya uchaguzi,” alisema Sheikh Mhinga.
Aidha, alisema baada siku 90 kumalizika fomu za kugombea zitatolewa kwa wagombea ambao watatoka miongoni mwa Baraza la Ulamaa ambao watachujwa mpaka kubaki mmoja kati yao.
WANAOWEZA KUMRITHI
Baraza la Ulamaa ambalo ndilo litakalotoa Sheikh Mkuu mpya wa Tanzania linaundwa na Kadhi Mkuu, Sheikh Abdallah Mnyasi na manaibu wake, Sheikh Abubakar Zubeir na Sheikh Ali Muhidin Mkoyogole.
Wengine ni  Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Salum Fereji, Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Makusanya, Sheikh wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Kiburwa na Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hamid Masoud Jongo.  
DUA YA KUMUOMBEA DAR
Awali asubuhi ya jana kabla ya mwili kusafirishwa kwa ndege kwenda Shinyanga kwa mazishi, viongozi wa serikali na vyama vya siasa akiwamo Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Mohamed Bilal, wamejumuika na waumini wa kiislamu kwenye Makao Makuu ya Bakwata kwenye shughuli ya kumsomea dua Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Simba.
Akizungumza na waandishi wa habari katika shughuli hiyo, Dk. Bilal alisema taifa limepoteza kiongozi muhimu wa kidini na kijamii na kidini na kwamba alikuwa kiungo muhimu kati ya viongozi wa dini na wa serikali na wa madhehebu ya dini nyingine.
“Tumepoteza kiongozi muhimu katika jamii na dini kwani alijenga maelewano kati ya viongozi wa dini na serikali,” alisema Dk. Bilal.
Aidha, alisema Mufti Simba alipenda watu wa dini zote na hakuwa mbaguzi na kuitaka jamii imuenzi kwa matendo yake mema.
Mbali na Dk. Bilal viongozi wengine na watu mashuhuri waliohudhuria ni Rais wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika (O.A.U), Dk. Salim Ahmed Salim, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, Mbunge wa Ilala, Idd Azzan Zungu, Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi.
Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Abood, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale Mwiru, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba. 
MABALOZI WAHUDHURIA
Mabalozi wa nchi za nje nchini Tanzania waliojumuika ni Balozi wa Comoro, Dk. Ahmada El Mohamed, Balozi wa Iran, Mehdi Aghasafari, Balozi wa Palestina, Dk. Nasri Abu Jaish na Balozi wa Sudan, Dk. Yassir Ali.
ANAVYOKUMBUKWA
Azzan alisema Mufti Simba alikuwa mtu wa karibu wa wabunge wa mkoa wa Dar es Salaam na kwamba kila walipokutana na kiongozi huyo aliwaasa kuwajali maskini.
Naye Prof. Lipumba alisema kiongozi huyo alipenda kuunganisha Watanzania wa dini mbalimbali, muadilifu na asiyependa makuu.
“Natoa pole kwa Watanzania wote taifa limepoteza kiongozi muunganisha watu, waamini wa dini zote njia ya kumuenzi ni kufuata yale yote mema aliyoyatenda yeye ametangulia sisi tuko nyuma,” alisema.
Naye Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, alionyesha kusikitishwa na kifo hicho, akisema Mufti Simba alikuwa rafiki yake wa karibu na mtu anayejali watu kwa matendo yake mema.
“Nimesikitishwa sana na kifo chake alikuwa rafiki yangu wa karibu, mpenda watu mimi ni mmojawapo ataendelea kuishi rohoni mwangu sababu ya matendo yake mema,” alisema Dk. Mengi.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Menomite, Dk. Steven Mang’ana, alisema kiongozi huyo hakuwa na hila na mtu bali alikuwa muunganisha watu na msimamia upendo na amani. 
Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi, Sheikh Kiburwa, alisema mwili wa marehemu ulisafirishwa jana kwa ndege kuekelea nyumbani kwake Majengo, mkoani Shinyanga ambako alizikwa saa 10 jioni.
Marehemu Mufti Simba alizaliwa Agosti 22, 1936 wilayani Magu, mkoa wa Mwanza na ameacha mke na watoto 
Na nipashe11. Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, amina.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni