MMILIKI WA BLOG HII

MMILIKI WA BLOG HII
TANGAZA NASI MATANGAZO YA KIJAMII BURE KUPITIA BLOG HII

Ijumaa, 11 Desemba 2015

MADIWANI ACHENI KUJITUKUZA


 MKUU wa mkoa wa Simiyu,Elaston Mbwilo amewataka madiwani wa
halmashauri ya wilaya ya Meatu mkoani humo kuacha tabia ya kujikuza ya
kujiita Mheshimiwa diwani kwani kufanya hivyo ni kujenga tofauti kati
yao na wapiga kura wao.

Pia Mkuu huyo amewataka madiwani wanaotokana na vyama vya upinzani
kutoona vibaya wala kichefuchefu kusimamia Ilani ya chama tawala (CCM)
kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi.

Akizindua kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo
muda mfupi baada ya kuapishwa na kumchagua Mwenyekiti na Makamu wa
Halmashauri hiyo jana katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya
wilaya ya Meatu alisema madiwani hawana budi kuepuka tabia ya
umangimeza mbele ya wananchi.

“Epukeni kujisikia kwa kujiita waheshimiwa huo ni ubinafsi mbele ya
wananchi bali kuweni na tabia na kujiwekea ratiba ya kuwatembelea
wananchi ili kupata mawazo yao bila kujali itikadi zao”alionya Mkuu
huyo.

Kuhusu falsafa ya “Hapa kazi tu” alisema kuwa kila diwani kwa
kushirikiana na wataalam wa halmashauri hiyo lazima kuwajibika kikamilifu ili
kuleta maendeleo ndani ya jamii.

Alionya tabia ya ubinafsi katika kupanga mipango ya mgawanyo wa
matumizi ya fedha za miradi na kamwe wasishiriki kujiingiza katika
ukandarasi na kuomba zabuni ndani ya halmashauri na badala yake watumie
fursa waliyo nayo kuunga mkono juhudi za halamashauri na wananchi.

“Ni marufuku kwa diwani kujiingiza katika kazi za ukandarasi na
uzabuni wa aina yoyote na iwe ni mwiko kwa diwani au kumtumia
mke,mtoto au ndugu yake kushiriki katika kandarasi ndani ya
Halamashauri,alisema.

Aidha aliwataka madiwani kuwa waaminifu katika matumizi ya fedha za
halmashauri kwa lengo la kujinufaisha kwa maslahi binafsi na kuwa omba
omba wa posho kila wanapoziendea ofisi za halmashauri.

“Madiwani hawaruhusiwi kujingiza katika kuomba zabuni ndani au katika
halmashauri yoyote nchini na ni mwiko iwe ni marufuku kwa madiwani
kuwa wazurulaji na wapiga porojo katika ofisi za halmashauri bali kwa
muda na mahitaji sahihi ya kufika katika ofisi za
watendaji”alisisitiza

Mkuu huyo pia aliwataka madiwani ndani ya mkoa wa Simiyu kuacha
kuingilia maamuzi halali ya kisheria kwa wananchi wao kuwazuia
kushiriki shughuli zozote za maendeleo kwa kudai kuwa anawatetea
wananchi wake.

“Kwa maana hiyo madiwani ninawaomba kuwa mfano na kuishi kwa taratibu
nzuri,epukeni ugomvi umwamba na ubabe mbele ya kadamnasi kwa kutumia
jina la uheshimiwa diwani”alisema.

Katika hatua nyingine UCHAGUZI wa kumpata Mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya ya Meatu umemalizika huku diwani wa Kata ya Ngoboko,Pius
Machungwa (CCM)akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo kwa
kipindi cha miaka 20.

Msimamizi wa Uchaguzi Chenya Ndaki ambaye pia ni Katibu tawala wa
wilaya hiyo alimtangaza Machungwa kwa kupata kura 31 na kumshinda
mpinzani wake James Kazangula(Chadema)aliyepata kura 11.

Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti,Juma Mpina(CCM) alitangazwa mshindi
kwa kupata kura  31 na kumshinda Zakayo Sanya(Chadema)ambaye ni
mlemavu wa ngozi aliyepata kura 11 .

                      NA HARUA UJUKU

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni